Tuesday, February 25, 2014

Nyumba ndogo Mmh

Jamani mwenzenu nashindwa kabisa kuelewa kwa nyie wanaume.



Mwanamume umeoa na mmejaaliwa watoto mashaallah,  tena huenda mmeanza maisha ya dhiki ya chumba kimoja kama stoo, maana kitanda, jiko, sturi, meza, gunia la mkaa, ndoo za maji, baiskeli kama ipo mpaka kopo la chooni na brash ya kuogea humo humo.

Anavumilia dhiki mdada wa watu nawe unamwimbia nyimbo za subira huku maharage, dagaa, mchicha, sukuma wiki, ndio mboga masikini 2000 anapanga matumizi ya siku nzima.

Mungu anawajaalia kipato mnajenga nyumba yenu, mnanunua fenicha, gari ya kutembelea, maisha yanakuwa mazuri mashaallah.
Mwanamke anaona huu ndio wakati wa yeye nae ajiringe kwenye nyumba yake baada ya kuteseka kwenye nyumba za kupanga.

Heee mwanamume ndio unaanza uesharati, nyumba ndogo, mkeo humuheshimu kila siku unarudi usiku wa manane, matumizi haba, gari anaishia kuiosha, ukiulizwa unajibu fedhuli na kumuona mshamba hafai kuitwa mkeo. 

Hivi huwa ni akili zenu, makusudi au kuzidiwa maarifa?

Unakuwa nyumbani kwako ukiingia kama kunawaka moto, mkeo na watoto wanajuta,  huna maongezi mazuri kwa mkeo wala watoto, ukirudi kazini ni kukoga na kutoka mpaka usiku wa manane.


Ole wake mkeo akuulize jambo utamtolea maneno machafu na kumuona si mwanamke tena.
Inafikia nyumba ndogo anakuja mtukana mkeo nawe unamtetea na kumgandamiza mkeo, hujui kama unawaathiri hata watoto. 
Wanashindwa kuzingatia masomo kutokana na tabia zako mbaya unazofanya mbele ya watoto.

Usifikiri watoto wote wanaofeli hawana akili wengine mazingira ya majumbani yanachangia sana kuwafelisha.
Kila siku ugomvi mara umempiga mama yao , matusi ndio usiseme, huduma mbovu, watoto mpaka wanaenda shule sare zimechanika huna habari, eeh hivi we ni mume au gume gume.




Ndio utakuta hukawii kupata matatizo kazini, mara umesimamishwa au kufukuzwa kazi unarudi unajipweteka nyumbani nyumba ndogo inakutoa mbio.

Huyo huyo ulokuwa unamtukana ndio utamtegemea masikini auze vibiashara , au alikuta labda kaweka kagenge nyumbani ndio kalishe familia.

Nyumba ndogo inaendelea kuwabamiza wengine we hata hakujui na jina keshasahau looh.

Umasikini mwingine tunauzalisha wenyewe  kisha tunamsingizia Mungu

Ni hayo tuu.






Toa maoni yako

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako